Naomba niweke wazi kwamba hapa hatufundishani kuwa jeuri kwenye mapenzi, isipokuwa hili ni somo la kumjengea moyo wa ukombozi yule anayenyanyaswa kwenye mapenzi. Wanyanyasaji ni wengi, hivyo ni vema wadhibitiwe.
Lazima
uwe makini kwa sababu hujui huyo anayekutenda malengo yake ni nini. Sasa basi,
kama dhamira yake ni kukuumiza na unapomuonesha kwamba kweli umeumia, unakuwa
umemfanya ajione amefanikiwa. Hii ndiyo sababu ya kukutaka usikubali kuonesha udhaifu
wake kwake. Atakwenda kuwakenulia wenzake.
Hata
kama una moyo mdogo mpaka unaingia kwenye kundi la akina ‘mahaba niue’,
hakikisha udhaifu huo rafiki mnafiki hauoni. Lia ndani peke yako, akitokeza
jikaushe. Akikuuliza mbona macho mekundu mjibu kwamba ulikuwa umelala kisha
tabasamu halafu mwambie, “usijali sweetheart, lete stori nyingine.”
Ni
falsafa ya kukuwezesha kupata alama A kwenye mapenzi. Kama ambavyo kanuni
inakwambia usimuoneshe adui yako udhaifu ulionao, ndivyo ambavyo na rafiki
mnafiki unavyotakiwa kumkabili. Hakupendi, kwa hiyo siyo mtu mwema kwako, hana
tofauti na adui.
Kwa
faida yako, uimara wako kwa mwenzi ambaye haoneshi kukujali, unaweza kumbadili
kutoka alipo hadi kuwa mpenzi bora wa maisha yako. Atabadilika pale tu
atakapogundua kwamba wewe ni mtu makini na huhitaji kuchezewa.
Atabadilika
pale atakapogundua kuwa wewe ni moyo wa chuma. Mwenye malengo ya kukucheza
shere halafu akakutana na kisiki cha mpigo, humfanya afikirie mara mbili, fikra
hizo humzalishia mawazo, anapokuwaza sana mwisho huumia. Unaona sasa, alitaka
kukuumiza lakini kaumia yeye.
FAIDA NI IPI SASA?
Maumivu
anayoyapata ndiyo yatakayomfanya ajirudi. Atakuheshimu na mwisho atakuonesha
upendo wa dhati. Sasa wewe shika hili, anapoanza kukuonesha upendo, upime kwa
umakini wake halafu jiridhishe kama kweli ana vigezo vya kumfungulia moyo.
Sikushauri
ukimbilie kumuacha mpenzi asiyeeleweka, kwani inawezekana akawa ndiye mpenzi
bora ila anasumbuliwa tu na mapepe. Siku zote usilaumu uhusiano, tambua kwamba
mpenzi mzuri atakupa furaha ya maisha na mpenzi mbaya ni changamoto ya kukupa
uzoefu.
Kadiri
atakavyokuona unajitambua ndivyo naye atakavyokuheshimu. Hebu mwache akwambie
“I am sorry”, halafu mjibu kwamba hujamuelewa, kwa hiyo aende halafu arudi
akiwa ana majibu ya kuridhisha ni kwa nini amekukosea. Muoneshe kwamba hutaki
mchezo, kwani unaweza kumuacha wakati wowote kama hatakuheshimu.
Tabia
ya unyonge kwa mpenzi wako, inaweza kumfanya akakuona wa bei rahisi mpaka
akakutambulisha kwa mpenzi mwingine, akiamini huna la kufanya. Yupo ambaye
alilazwa kitanda kimoja na mwanamke mwenzake, naye kwa sababu ni mahaba niue,
akaogopa kumwacha mwanaume, eti anampenda sana.
Yupo
mwanamke aliyemtambulisha mumewe kwa mwanaume wake mwingine, halafu mume badala
ya kuchukua uamuzi, akakimbilia kulalamika kwa wakwe na mshenga. Jenga kitu
kwamba unapolalamika sana, watu wanakuona dhaifu, hebu chukua uamuzi kwa ajili
ya maisha yako ya leo na kesho.
KATAA
KUWA MAHABA NIUE
Kila
mtu anatakiwa ayaheshimu mapenzi. Hakikisha mwandani wako anakuwa upande wako
kila siku. Mpenzi bora anapimwa kwa vitendo vyake. Je, anajali furaha yako?
Anazingatia ujenzi wa maisha yako? Ni kwa namna gani anahakikisha unafurahi na
anajengaje maisha yako?
Majibu
chanya ya maswali hayo, yakupe sababu ya kuwa naye kwa moyo mkunjufu. Endapo
uhusika wake hautakuridhisha, anza kutumia njia ambazo zitamfanya akuheshimu.
Siku zote unatakiwa ujiheshimu mwenyewe halafu na wengine ndiyo wakuheshimu.
Ukijionesha ni bei rahisi hakuna atakayekuona bei yako ni ghali.
Hivyo basi, ukikubali kujionesha wewe ni mahaba niue, yatakuua kweli. Huyo
utakayemlilia, hawezi kukuhurumia, badala yake utampa pointi ya kwenda kujisifu
kuwa amekupata na umekamatika kwake huna ujanja wowote.
0 maoni:
Chapisha Maoni