Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) limemteua Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya soka ya FIFA kwa miaka
minne ijayo. Uteuzi huo unaanza mwaka huu 2017 hadi 2021.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo ya Januari 18, 2017 iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa
FIFA, Fatma Samoura inasema: “Tuna faraja kukufahamisha kuwa umeteuliwa
kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya FIFA. Tunachukua nafasi hii
kukupongeza kwa uteuzi huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo ilifafanua kuwa Kamati hiyo inayoongozwa na Sheikh Salman Bin
Ebrahim Al Khalifa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Bara la Asia,
ina majukumu ya kusimamia mipango ya maendeleo ya mpira wa miguu duniani
kote.
Wajumbe wengine wote watatangazwa kwenye tovuti ya FIFA ambayo ni www.FIFA.com.
Huu ni mfululizo wa Tanzania kupata nafasi katika vyombo vikubwa
vinavyoendesha soka FIFA na CAF. Mwishoni mwa mwaka jana, CAF –
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika lilimteua Rais Malinzi kuwa mmoja wa
wajumbe wa kamati maalumu inayoongozwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou ya
kuboresha mfumo wa uongozi wa CAF.
TFF inamshukuru Rais Gianni
Infantino na kamati yake ya ushauri kwa kumteua Malinzi katika nafasi ya
ujumbe katika kamati hiyo muhimu ya maendeleo ya soka ulimwenguni.
0 maoni:
Chapisha Maoni