Na Alex Mwenda
KOCHA wa Simba SC, Joseph Marius Omog amefurahishwa na hali ya kujituma ya wachezaji wake katika mechi mbili za mwanzo za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na amewataka waendelee hivyo.
Simba ilishinda mechi ya pili mfululizo ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu juzi baada ya kuichapa JKT Ruvu 1-0, bao pekee la kiungo Muzamil Yassin katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ilishinda mchezo huo ikitoka kushinda 2-0 katika mchezo wake wa kwanza wa mzunguko wa pili dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara mabao ya Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na Muzamil Yassin.
Kocha wa Simba SC, Joseph Marius Omog amefurahishwa na hali ya kujituma ya wachezaji wake katika mechi mbili zilizopita
Na baada ya mechi hizo mbili, Omog amewapongeza wachezaji wake kwa hali ya kujituma wanayoionyesha na kuwataka waendelee hivyo hivyo ili mwisho wa msimu watimize ndoto za kutwaa ubingwa.
Omog pia alitoa pongezi za kipekee kwa mshambuliaji mpya, Pastory Athanas aliyeonyesha kiwango kizuri Jumamosi na kuseti bao pekee lililofungwa na Muzamil.
Baada ya ushindi wa juzi, Simba imefikisha pointi 41 kufuatia kucheza mechi 17 ikiendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 37 za mechi 17.
Simba itashuka tena dimbani Alhamisi wiki hii kumenyana na Ruvu Shooting ya Pwani Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
0 maoni:
Chapisha Maoni