Pages

Ijumaa, 20 Januari 2017

Aishi Manula alivyosimama langoni bila kufungwa

Mmoja wa wachezaji waliotia fora kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi mjini Zanzibar ni kipa wa Azam, Aishi Manula.

Image result for Aishi Manula
Si tu kwamba ameisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa huo. Lakini pia amecheza mechi zote za michuano hiyo bila kuruhusu goli. Alisimama langoni kwa dakika 450 bila kuruhusu nyavu zake kuguswa.
Manula, alichaguliwa kuwa kipa bora wa michuano hiyo, akimzidi kidogo kipa wa Simba, Daniel Agyei aliyeruhusu bao moja, ambalo alifungwa na beki wake, Novatus Lufunga.

Mechi yake ya kwanza kukaa golini ilikuwa dhidi ya Zimamoto na Azam kushinda bao 1-0, mechi ya kundi B. Mechi iliyofuata ililazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya timu kibonde ya Jamhuri ya Pemba.

Manula aliendelea kudhihirisha kuwa si kipa wa mchezo mchezo, aliposimama langoni kwenye mechi ngumu dhidi ya Yanga bila kuruhusu bao, Azam ikishinda mabao 4-0.
Tayari alikuwa ameshacheza dakika 270 bila kuruhusu goli. Kwa matokeo hayo, alikuwa ameipeleka timu yake nusu fainali ikiwa imekamata nafasi ya kwanza, hivyo ikacheza na mshindi wa pili kwa kundi A, Taifa Jang’ombe. Kwenye mechi hiyo, Azam ilishinda bao 1-0 na kwenda moja kwa moja, fainali dhidi ya Simba.
Image result for Aishi Manula







Katika mechi ya fainali, Manula hakuweza kuruhusu timu yake kufungwa iliposhinda bao 1-0 na kutwaa kombe hilo kwa dakika 450 alizosimama langoni.
Mchezaji huyo alijiunga na Azam FC akitokea mkoani Morogoro,  alisajili katikati ya mwaka 2012 akiwa na miaka 17 baada ya  kuonesha uwezo mkubwa katika michuano ya Taifa ya vijana, Copa  Coca Cola akiwa na kombaini ya Mkoa wa Morogoro.


Kocha mkuu wa Azam wakati huo Boris Bunjak alianza kuvutiwa na uwezo wa kijana huyo, akaanza kumtumia kwenye baadhi ya michezo wa Ligi Kuu msimu wa 2012/13.

“Nakumbuka makocha wa kikosi cha pili cha Azam, makocha waliniona na kuvutiwa na mimi kwenye mechi za Kombe la Uhai mwaka 2012, ndipo walipoanza kunipa baadhi ya mechi za Ligi Kuu,” anasema Manula na kuongeza.

“Kusema kweli hili la kuachiwa baadhi ya mechi nikiwa na makipa hawa kulichangia kunijenga na kujiamini,” anasema kipa huyo.
Kwa kawaida mchezaji yoyote kwenye klabu nyingine ikiwemo hata Azam anapong’ara anatarajiwa zaidi kwenda kujiunga na klabu kubwa zenye mashabiki wengi nchini za Simba na Yanga, lakini Manula ana mawazo tofauti kabisa.

“Hapana, nipo mahali sahihi katika wakati sahihi na ndoto yangu ni kucheza katika klabu sahihi. Nilijiunga na timu hii nikiwa mwanafunzi wa kidato cha pili na wamenifanyia mambo mengi hata nje ya mpira,” anasema kipa huyo na kuongeza.

“Nipo katika klabu ambayo inamfanya  mchezaji awaze kucheza mpira tu, kuna kila kitu muhimu kwa mchezaji, hosteli nzuri ambayo ina kila kitu, kuna TV katika kila chumba jambo ambalo linamfanya mchezaji kutumia muda  wake wa mapumziko kutazama mpira kwa lengo la kujifunza zaidi.

  Gym ya uhakika, mishahara mizuri kwa wachezaji, na malengo  ambayo inafanya mchezaji yoyote kucheza katika  timu hii, nitoke hapa niende wapi?,” anasema kipa huyo kijana, akiwa kwa sasa ni tegemeo kwenye timu ya taifa, Taifa Stars.

0 maoni:

Chapisha Maoni