Na Alex Mwenda
Kamati
ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limepitisha ombi la
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) la Zanzibar kuwa mwanachama
kamili wa CAF. Katika kikao chake cha Kamati ya Utendaji kilichoketi
Januari 12, mwaka huu kiliamua kupitisha ombi hilo kuwa moja ya ajenda
za Mkutano Mkuu wa CAF utakaofanyika Machi 16, 2017 huko Addis Ababa,
Ethiopia.
Hivyo
sasa Mkutano Mkuu huo utapiga kura na kama Zanzibar itapata idadi ya
kura theluthi mbili yaani 2/3 ya wanachama wote, itatangazwa kuwa
mwanachama mpya kamili wa CAF ambako atakuwa na haki mbalimbali za kama
mwanachama.
Haki
hizo ni pamoja na kushiriki michuano yote inayoandaliwa na kusimamiwa
na CAF na hii ni pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), fainali
za Afrika Wanawake (AWCON), fainali za vijana (AFCON U17 na AFCON 20)na
pia kuhudhuria mikutano mbalimbali ya CAF kama mwanachama kamili,
kupokea na kusimamia kozi mbalimbali za CAF nakadhalika.

Pia
itakuwa na fursa ya kupiga kura katika masuala muhimu ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Afrika (CAF) tofauti na sasa ambako inapata fursa ya
klabu zake zinazoshika nafasi ya juu katika Ligi Kuu ya Zanzibar
kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa Mheshimiwa Nape
Nnauye – Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya
Muungano Tanzania pamoja na Mheshimiwa Rashid Ali Juma - Waziri wa
Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanizbar
(SMZ) kwa kufanikisha hatua hiyo.
Pia,
TFF inatoa shukrani kwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar
(ZFA), Ravia Idarus Faina pamoja na Rais wa Heshima wa TFF Leodegar
Chilla Tenga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa CAF na Marais
wa Heshima wa TFF Said Hamad El Maamry ambaye ni Mjumbe wa kudumu wa
CAF na Mzee Muhiddin Ndolanga na wadau wote wa familia ya mpira wa miguu
kwa mafanikio ya hatua hii.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa sasa linajikita kwenye kampeni
nzito ya kuomba kura za kutosha kuhakikisha kwamba Zanzibar inapata
nafasi hiyo ya uanachama kamili.
Kadhalika
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia viongozi wake wako
kwenye mchakato wa kumfanyia kampeni Rais wa Heshima wa TFF, Bw.
Leodegar Chilla Tenga kuhakikisha anashinda nafasi ya Ujumbe wa Kamati
ya Utendaji (Council) ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA).
Leodegar
Tenga anawania nafasi hiyo kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha
ya Kiingereza akishindana na Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu la Zambia, Kalusha Bwalya na Kwesi Nyantakyi wa Ghana.
TFF inaomba Watanzania wote na wadau wote wa mpira wa miguu nchini kutuunga mkono katika juhudi na jitihada zetu za kuona Zanzibar inapata nafasi hiyo kadhalika Tenga anakuwa mjumbe kwenye baraza la ushauri huko FIFA.
0 maoni:
Chapisha Maoni