Pages

Jumamosi, 17 Desemba 2016

Ajinyonga kwa katani kisa ugumu wa maisha

Watu wawili wamekufa katika matukio tofauti mkoani Rukwa, likiwamo la mmoja kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani kwa madai ya ugumu wa maisha.


Katika tukio la kwanza lililotokea usiku wa kuamkia juzi, mkazi wa kijiji cha Chipu Manispaa ya Sumbawanga, Ignas Mambi (52) alijiua kwa kujinyonga.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Deus Masanja, alisema chanzo cha kujiua kwa mtu huyo kinadhaniwa kuwa ni ugumu wa maisha.
Alisema mara kwa mara marehemu alikuwa akilalamikia ugumu wa maisha, huenda ndiyo sababu inayodhaniwa kuchukua uamuzi mgumu na kujinyonga porini katika mti kwa kutumia kamba ya katani.
Katika tukio la pili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, alisema lilitokea Desemba 13, saa tano asubuhi katika kijiji cha Kanyezi, wilayani Kalambo.
Katika tukio hilo, Kamanda Kyando alisema bibi kizee Noelia Pintilila (80) aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.
Kyando alisema mtuhumiwa baada ya kutenda kosa hilo, alikimbia kusikojulikana na kwamba alimuua bibi huyo kutokana na kuwa mtuhumiwa alikuwa akianguka kifafa na mara kwa mara alikuwa akimtuhumu bibi huyo kuwa ndiye anayemloga.
Kutokana na kitendo hicho, Kyando aliwasihi wananchi wa mkoa huo kuachana na imani za kishirikina na kujichukulia sheria mikononi kwa kuwa zimekuwa chanzo cha vifo vya watu wengi.
Soucre: Nipashe

0 maoni:

Chapisha Maoni