POLISI mkoani Morogoro wakishirikiana na kikosi kazi cha taifa cha kupambana na dawa za kulevya wamekamata tani tano za bangi, mbegu zake zaidi ya kilo 300 na nyara za serikali yakiwemo magamba 42 ya mnyama adimu kakakuona.
Watu wawili wamekamatwa kuhusu sakata hilo. Watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni maalumu kuanzia Desemba 16 hadi 19, mwaka huu katika wilaya ya Kilosa na Mvomero.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, (SACP), Ulrich Matei, amesema jana kuwa, Polisi wa mkoa, na timu maalumu ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya kitaifa ikiongozwa na SACP, Mihayo Msikhela wamewakamata watuhumiwa Ally Rashid Abdallah Manji (36) na Julius Keneth (40).
Amesema, Manji alikamatwa Desemba 19, mwaka huu majira ya saa tatu asubuhi maeneo ya Kipara, kijiji cha Msengele, Kata ya Doma, Tarafa ya Mlali, wilaya ya Mvomero kwa kushirikiana na kikosi cha kudhibiti dawa za kulevya taifa.
Walipompekua mtuhumiwa huyo ambaye ni mkulima na mkazi wa Doma alikutwa akiwa na bangi viroba 11 vyenye uzito wa kilo 800 ambapo vitano vilikuwa na mbegu na vingine sita vikiwa na bangi yenyewe.
Kamanda Matei alisema katika upekuzi wa kibanda hicho mtuhumiwa huyo pia alikutwa na nyara za serikali bila kuwa na vibali vyovyote.
Nyara hizo ni ngozi ya fungo na magamba 42 ya kakakuona.
Katika operesheni iliyofanyika pia Desemba 17, mwaka huu saa tatu asubuhi katika bonde la Msimbalenga Polisi wa mkoa kwa kushirikiana na timu hiyo walifanikiwa kumkamata Julius Keneth (40), mkulima na mkazi wa kitongoji cha Mkuruzi, kijiji cha Madudumizi, kata ya Zombo, wilayani Kilosa, mkoani humo.
Mtuhumiwa huyo alikutwa akimiliki shamba la bangi lenye ukubwa wa ekari 20 na walilitekeleza na moto.
Amesema, katika upekuzi wa kibanda kilichopo katika shamba hilo walifanikiwa kukamata bangi iliyokuwa imehifadhiwa kwenye mifuko mitatu ya sandarusi tayari kwa kusafirishwa.
Alisema Desemba 19, 2016 saa nne asubuhi , maeneo ya Kipera, kijiji cha Msengele, kata ya Doma, Tarafa ya Mlali wilaya ya Mvomero, timu hiyo ilinasa viroba 61 vya bangi vilivyokadiriwa kuwa na uzito wa kilo 4,900 kutoka kwenye nyumba inayomilikiwa na mtu aliyatajwa kwa jina la Bulumo ambaye pia alikamatwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni