MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha imeruhusu maombi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kukata rufaa ya kuomba dhamana yake ndani ya siku 10 kuanzia jana. Wakati mahakama hiyo ikiruhusu hilo, tayari mawakili wa Lema wamesajili rufaa namba 126/2016 katika mahakama hiyo jana jioni.
Awali akizungumza kuhusu ruhusa hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Dk Modesta Opiyo alisema hakukuwa na ucheleweshwaji wowote wala ukiukwaji wa sheria kwa mawakili wa Lema, walioufanya wakati wa uwasilishaji wa maombi ya kuongezewa muda wa kukata rufaa.
Akisoma uamuzi wa kama maombi hayo ya Lema yalikuwa ndani ya muda au la, Jaji Opiyo alisema maombi hayo yalikuwa ndani ya muda kwa sababu mawakili wa serikali walihesabu siku hadi za mwisho wa wiki (Jumamosi na Jumapili).
Alisema hakukuwa na uvunjaji wa sheria, uliofanywa na mawakili wa mbunge huyo, bali mawakili wa serikali wao waliweka pingamizi zao wakahesabu hadi siku za mapumziko.
"Mahakama hii imemruhusu Lema kukata rufaa ndani ya siku kumi kuanzia leo hii, pia busara ya mahakama ni lazima iangaliwe katika kuamua jambo hili la uamuzi wa rufaa hii, hivyo mawakili wa Lema hawakuwa nje ya muda kama ilivyodaiwa na mawakili wa serikali," alisema.
Akichambua hoja za mabishano ya kama nia ya notisi ya kukata rufaa ilipitiliza muda wake au la Jaji Opiyo, alisema awali alitupilia mbali pingamizi wiki iliyopita baada ya kupitia hoja za pande zote.
Alisema kuwa pingamizi hizo za serikali, walizokuwa wakitaka maombi hayo yasisikilizwe kuwa mawakili hao hawakuwa na hoja za kisheria zenye mashiko.
Maombi hayo namba 69, upande wa serikali ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Hashim Ngole, Matenus Marandu, Elizabeth Swai na Adelaide Kasala huku Lema akitetewa na wakili, Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.
Akiwasilisha hoja za maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi hiyo ili rufaa hiyo iweze kusikilizwa, Wakili Mfinanga alidai mahakamani hapo kuwa maombi hayo, yamewasilishwa mahakamani hapo chini ya Kifungu 361(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Alidai kuwa maamuzi wanayotarajia kukatia rufaa ni uamuzi uliotolewa Novemba 11 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
0 maoni:
Chapisha Maoni