MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesikitishwa na klabu yake, KRC Genk kumfukuza kocha Mbelgiji Peter Maes.
Akizungumza na GIMMIE CHURCHBOY leo kwa simu kutoka Ubelgiji, Samatta amesema kwamba amesikitishwa na taarifa hizo, lakini hana namna nyingine zaidi ya kukubali matokeo.
"Siyo taarifa nzuri kwa mtu ambaye alitokea kuniamini kwa muda mfupi, lakini hakuna chaguo zaidi ya kuendelea kujituma na kuwa bora zaidi, ili kumpendeza kocha atakayekuja,"amesema Samatta.
Mbwana Samatta alisajiiwa na Peter Maes Genk
Akimzungumzia zaidi Maes, Nahodha huyo wa Tanzania alisema; "Alikuwa kocha kocha mzuri, aina ya ufundishaji wake ulikuwa wa moja kwa moja na alikuwa rafiki kwa kila mchazaji,".
Genk imemfukuza rasmi Maes leo baada ya matokeo mabaya ya hivi karibuni na kuelekea mchezo wa kesho, aliyekuwa Msaidizi wake, Rudi Cossey ataiandaa timu.
Maes ndiye aliyemsajili Samatta Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na akamuamini haraka na kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Chini ya Maes, Samatta amecheza mechi 35 Genk,18 msimu uliopita na 17 msimu huu na kati ya hizo, ni michezo 17 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na saba msimu huu.
Mechi 18 kati ya hizo alitokea benchi, nane msimu uliopita na 10 msimu huu, wakati nane hakumaliza baada ya kutolewa, sita msimu uliopita na mbili msimu huu huku akiwa amefunga jumla ya mabao tisa, manne msimu huu na matano msimu uliopita.
Maes alijiunga na Genk msimu wa 2015-2016 kutoka KSC Lokeren na ameiongoza timu hiyo katika mechi 81 rasmi.
Genk kesho itacheza na KAA Gent ikiwa chini ya kocha wa muda, Mbelgiji pia, Rudi Cossey na klabu imemshukuru Peter Maes kwa kazi yake nzuri kwa kipindi chote alichokuwa na timu na kumtakia kila la heri aendako.
0 maoni:
Chapisha Maoni