Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kulipa madeni ya
Watumishi na tayari imelipa jumla ya sh. bilioni 29 kwa watumishi
mbalimbali wa umma wakiwemo walimu ikiwa ni sehemu ya madeni yao.
Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Januari 21, 2017
wakati akizindua vyumba vitatu vya kisasa vya madarasa katika shule ya
sekondari Iwawa iliyoko wilayani Makete, amesema kuwa Serikali
imedhamiria kumaliza madeni ya watumishi hao, ambapo hadi kufikia
Novemba mwaka jana jumla sh. bilioni 29 zililipwa kwa watumishi 31,000.
Majaliwa amesema kwa sasa Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna
madeni mapya yanayozalishwa hivyo amewataka watumishi wa umma na
wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali.
Hata hivyo alisema Serikali inaendelea na mikakati ya kuboresha sekta
ya elimu kwa kujenga mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.
“Tumeanza mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu katika halmashauri nchini.
Hapa Makete tumeleta sh. milioni 557 kwa ajili ya ujenzi huo,” amesema.
Amesema kuwa Serikali inafanya jitihada za dhati za kuhakikisha kila
Mtanzania anapata elimu kwa kuwa elimu ni kichocheo cha maendeleo ya
jamii. “Tumedhamiria kumpatia elimu kila Mtanzania, hivyo halmashauri
zihakikishe kila kijiji kinakuwa na shule ya msingi na lazima ziwe na
darasa la awali,” amesema.
Pia, Majaliwa ametimiza ahadi yake ya kumpatia laptop mwanafunzi Ally
Alijai wa Chuo kikuu cha SAUT tawi la Songea mkoani Ruvuma, kufuatia
ahadi yake aliyotoa mwanzoni mwa mwezi huu alipokuwa katika ziara yake
kikazi mkoani Ruvuma, lengo likiwa ni kuendeleza kipaji cha utunzi wa
vitabu kwa mwanafunzi huyo.
Amesema mwanafunzi huyo alionyesha umahiri mkubwa katika utungaji wa
kitabu ambacho kinaweza kutumika kufundishia katika shule za sekondari.
Aidha, Majaliwa amesema kuwa tayari kitabu hicho kimeshawasilishwa
Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) kuona kama kinaweza kuanza kutumika kwa
kufundishia. Mwanafunzi huyo alishukuru kwa zawadi hiyo na kuahidi
kutunga vitabu vizuri zaidi.
0 maoni:
Chapisha Maoni