Na Alex Mwenda
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa furaha
maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Utendaji ya CAF ya kuipa Tanzania
nafasi ya kucheza fainali za Afrika za vijana chini ya umri wa miaka 17
(Afcon U17). Mashindano haya yatanyika nchini Gabon kuanzia tarehe 21
Mei, 2017 hadi 04 Juni, 2017.
Timu nane zitashiriki fainali hizi na zimegawanywa makundi mawili,
kundi A ni Gabon, Ghana, Guinea, Cameroon na kundi B ni Mali, Niger,
Angola na Tanzania. Washindi wawili wa kila kundi wataliwakilisha bara
la Afrika katika fainali za dunia huko India mwezi Novemba mwaka huu.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linatoa shukrani za pekee kwa
Mh. Rais Dr John Pombe Magufuli kwa jitihada za Serikali kusapoti
michezo, tunamshukuru sana Mh. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim kwa
kutupa shime na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya timu. Shukrani kwa
Mh. Nape Nnauye na Wizara kwa ushirikiano wa karibu aliotupatia
wakati wote wa kuandaa timu na kuelekea kwenye mashindano hatua ya
mtoano.
Tunamshukuru sana Bw. Issa Hayatou Rais wa CAF na Kamati yake ya
Utendaji kwa kututendea haki, Bw. Leodeger Tenga Rais wa heshima wa TFF
na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF tunamshukuru na kumpongeza sana
kwa jitihada binafsi alizofanya kuhakikisha haki ya Tanzania haipotei.
Ninaishukuru sana Kamati ya Utendaji ya TFF, Chama cha Mpira Zanzibar
ZFA, Kamati ya Mpira wa Vijana ikiongozwa na Bw. Ayoub Nyenzi, viongozi
wa vyama vya mpira vya Mikoa, na Sekretariet ya TFF ikiongozwa na
Katibu Mkuu Bw. Mwesigwa Selestine kwa kazi kubwa waliyoifanya kusimamia
timu.
Tunamshukuru Dr. Paul Marealle mjumbe wa Kamati ya Tiba ya CAF na
Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya TFF kwa kufuatilia kwa karibu suala hili
na kutoa ushauri wa kitaalam kwa TFF.
Shukrani za pekee kwa washirika wetu Azam Media, Airtel, Coca Cola na
Kampuni ya SS Bakhresa. Mchango wao ni mkubwa katika kufikia mafanikio
haya.
Wazazi wa vijana wetu wa Serengeti Boys tunawashukuru kwa kuwaruhusu
watoto wao washiriki kwenye mashindano haya. Tunaomba waendelee na moyo
huo.
Pongezi nyingi sana kwa wachezaji wetu Serengeti Boys na benchi lao
la ufundi kwa kututoa kimasomaso na kuhakikisha bendera ya Tanzania
inapeperushwa Gabon mwezi Mei. Kazi kubwa mmeifanya, mmepambana na timu
kubwa na mkatoka mashujaa. Mmeiondoa Seycheles mashindanoni, mkaiondoa
timu kubwa ya Afrika Kusini mashindanoni na mkataoa sare ya jumla ya
mabao 3-3 dhidi ya Kongo na kutolewa kwa bao la ugenini. Wapinzani wetu
Kongo hawakutenda haki kwa kuchezesha wachezaji wakubwa kwa umri. CAF
walipowaagiza, si mara moja, ila mara tatu kuwa wamlete mchezaji husika
anayetuhumiwa kuzidi umri hawakufanya hivyo na wakatolewa mashindanoni.
Safari ya kwenda Gabon haikuwa fupi ilikuwa ndefu. Kufuatia maono ya
mbali ya TFF safari hii ilianza mwaka 2014 mara tu baada ya mashindano
ya Copa Coca Cola ambayo yalihusisha vijana umri chini ya miaka 15
wakati huo. Wachezaji bora katika mashindano hayo walikusanywa pamoja
wakawekwa kambini na kuanza mazoezi yaliyoambatana na ziara za mechi za
majaribio mikoani. Ni katika ziara hizi vipaji vipya vilionekana na
kuongezwa kwenye timu.
TFF inavishukuru sana vyama vya mpira vya India, Seychelles,
Madagascar, Rwanda na Korea Kusini kwa kufanikisha kambi za kimataifa za
Serengeti Boys. Kambi hizi zilitoa fursa kwa vijana wa Serengeti Boys
kupata uzoefu wa kimataifa kupitia michezo ya kujipima nguvu waliyocheza
dhidi ya timu kubwa duniani kama Marekani, Korea Kusini, Misri,
Malasyia, Madagascar na India.
Tunayashukuru sana makundi yote ya mashabiki wa timu zetu za Taifa
kwa kutoa hamasa wakati wote Serengeti Boys ilipocheza. Washiriki mbali
mbali kwenye mitandao ya jamii tunawashukuru kwa kufuatilia kwa karibu
maendeleo ya timu na kuwatia moyo vijana. Tuendelee na moyo huu.
Vyombo vya habari tunavishukuru sana kwa kutoa taarifa mbali mbali zinazohusu timu, kuandika makala na kuhamasisha vijana.
Sasa tunayo kazi kubwa mbele yetu, kuhakikisha Tanzania inarudi na
Kombe toka Gabon. Nimeliagiza benchi la ufundi liandae program ya
maandalizi ya timu kuelekea Gabon 2017. Program hii itahusisha kambi
ndani ya nchi (ambayo tayari imeanza) na kambi ya angalao mwezi mmoja
nje ya nchi, TFF iko mbioni kutafuta kambi hii na karibu tutafanikiwa
kuipata, itakuwa ni katika nchi iliyoendelea kisoka.
Serengeti Boys haina mdhamini. Gharama za maandalizi ni kubwa na
hazitapungua dola za kimarekani laki nne na zitajumuisha gharama za
mechi za majaribio (gharama za mechi hizi hazipungui dola 50,000.- kwa
kila mechi), gharama za kambi ndani ya nchi, gharama za kambi nje ya
nchi ambazo hazitapungua dola laki moja ($100,000), usafiri wa kwenda na
kurudi Gabon,gharama za timu wakati wa mashindano ikiwemo usalama wa
timu Gabon, pamoja na vifaa na matumizi mengine. TFF kupitia mfuko wake
wa TFF Football Development Fund itafanya kila jitihada kuhakikisha
pesa hizi zinapatikana ili kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri Gabon.
Hatutaki viwepo visingizio kama ambavyo huwa inatokea kwa nchi nyingine.
Tunatoa wito kwa Serikali, mashirika binafsi na umma, watu binafsi,
makundi mbali mbali ya jamii kwa pamoja tushirikiane tuhakikishe kila
kinachohitajika kinapatikana ili kuhakikisha mafanikio ya timu. Sekta ya
umma na ya binafsi karibu mtoe ushamini kwa Serengeti Boys ili nanyi
mkuze jina la biashara zetu. Bahati nzuri jina la Serengeti Boys
linachukua jina la moja ya vivutio vyetu vikubwa vya utalii, hii ni
fursa kubwa ya kutangaza jina la nchi yetu na vivutio vyake vya utalii
kupitia timu hii na fainali hizi za Afrika.
Fainali hizi za Afrika zitakuwa ni fursa pekee kwa wachezaji wa
Tanzania kuingia kwenye anga za Kimataifa. Wachezaji wengine wakubwa
duniani wakiwemo kina John Obi Mikel, Celestine Babayaro, Nwanko Kanu,
Kelechi Ihenacho, Samuel Kuffour, Nii Lamptey, Michael Essien wametokea
kwenye fainali hizi.
Ushiriki wa Tanzania katika fainali hizi itakuwa ni fursa ya pekee ya
kuwa hamasisha wadau wa mpira wa miguu Tanzania ili na sisi tuweze
kuanda fainali zijazo nzuri za Afrika za vijana chini ya umri wa miaka
17 mwaka 2019. Tanzania ni mwenyeji wa fainali hizi. Siku ya fainali ya
Gabon Afcon U17 kabla ya kombe kutolewa Tanzania tutakabidhiwa rasmi
utambulisho wa kupokea mashindano haya toka kwa Gabon .
Ninaomba nimalizie kuwaomba Watanzania wenzangu timu yetu ya
Serengeti Boys tuiweke kwenye sala na dua zetu ili izidi kupata
mafanikio.
Mungu ibariki Serengeti Boys.
Mungu ibariki Tanzania.
Mungu ibariki Afrika.
Ahsanteni sana.
Jamal Malinzi
Rais
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).






0 maoni:
Chapisha Maoni