Na Alexx Mwenda
Baada ya kufanikiwa kurudi katika mashindano ya Fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 17, timu ya
taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 imeandaliwa
kambi ya nje ya nchi kwa mara nyingine.
Katika mkutano na waandishi wa habari hii leo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kuwa kambi hio itakuwa ya muda usiopungua mwezi mmoja kwa ajili ya maandalizi ya Fainali hizo zilisogezwa mbele kwa muda wa mwezi mmoja na sasa zitafanyika kuanzia mwezi wa tano nchini Gabon.
” Lazima na sisi twende kitaalam. Tunakwenda kucheza na Mali, Angola na mataifa mengine yaliyo mbele yetu, ” Amesema Rais Malinzi na kuongezea kuwa takriban bilioni moja zitatumika kama gharama za maandalizi hayo zikiwemo mechi tatu za majaribio.”
” Hatutaki visingizio kama ambavyo imekuwa ikitokea. ”
Naye mshauri wa ufundi wa soka la vijana, Kim Poulsen amesema kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania imeanza kujenga bomba la mtiririko sahihi wa maendeleo ya vijana.
” kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikisaka mafanikio ya soka kwa kuanzia juu kwenda chini na mara zote imefeli. Kuna utofauti sasa na hii ndio njia sahihi, kuwekeza kwa kuanzia chini kupata bomba la mtiririko wa maendeleo ya soka nchini. ”
Poulsen ambaye ni mkuu wa benchi la ufundi la Serengeti Boys pia amezungumzia matarajio ya kufanya vizuri kwa kuwa maandalizi yanaenda vizuri.
” Tulianzia maandalizi India na tunataka kumalizia India kwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyikia huko. ” Amesema Poulsen.
0 maoni:
Chapisha Maoni